Skip to main content

Usalama wa Somalia muhimu kwa dunia nzima: Baraza la Usalama

Usalama wa Somalia muhimu kwa dunia nzima: Baraza la Usalama

Baraza la Usalama leo limehitimisha ziara ya siku moja nchini Somalia, kwa ajili ya kuonyesha mshikamano wake na nchi hiyo wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu mwezi Agosti mwaka huu.

Wakati wa ziara yao wajumbe wa baraza hilo wamekuwa na mazungumzo na Rais Hassan Sheikh Mohamud, Waziri Mkuu na viongozi wengine wa mikoa, wakisisitiza umuhimu wa kuhalalisha mchakato wa uchaguzi uliokubaliwa na wanasiasa awali mwaka huu.

Aidha wamezungumza na wawakilishi wa wanawake waliofikisha maombi yao ya kupewa asilimia 30 ya viti vya uwakili kwenye bunge lijalo.

Kiongozi mwenza wa ziara hiyo ni Mwakilishi wa kudumu wa Misri kwenye Umoja wa Mataifa Amr Abdellatif Aboulatta akieleza:

(Sauti ya Bwana Aboulatta)

“Kitu muhimu zaidi ni kusonga mbele na kuwa jumuishi. Bila hivyo, hatutaweza kupata amani kwenye nchi hiyo. Somalia na pembe ya Afrika ni muhimu kimkakati kwa dunia nzima, siyo tu kwa ukanda huo. Tunapaswa kusonga mbele. Tutaisaidia serikali hii ikitaka kujenga upya jeshi lake na uchumi wake, kila kitu.”

Wakati huo huo, taarifa iliyotolewa leo na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia UNSOM, imemnukuu mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini humo Michael Keating akisema jamii yote ya kimataifa inajali hali ya usalama nchini Somalia, na Umoja wa Mataifa unataka kuhakikisha uchaguzi ujao utafanyika kwa uhuru na usawa.