Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani kuuawa kwa walinda amani watano Mali

Ban alaani kuuawa kwa walinda amani watano Mali

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amelaani mashambulizi yaliyotokea leo nchini Mali na kusababisha vifo vya walinda amani watano kutoka Chad na kujeruhi wengine watatu.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wake imeeleza kwamba msafara wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa (MINUSMA) umepigwa kwa bomu lililotegwa ardhini kwenye eneo la Kidal kaskazini mwa nchi, na kisha ukashambuliwa na kundi la washambuliaji wasiojulikana.

Tangu mwanzo wa mwaka 2016, mashambulizi takriban 12 yamefanyika kwenye eneo hilo na kusababisha vifo vya walinda amani 12.

Katibu Mkuu ametuma salamu zake kwa familia za wahanga pamoja na serikali na raia wa Chad, akiwatakia nafuu waliojeruhiwa.

Aidha, ameomba watekelezaji wa uhalifu huo wapelekwe mbele ya sheria, akikariri kwamba mashambulizi dhidi ya walinda amani ni uhalifu wa kivita.