Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusipoteze fursa ya kujumuisha walemavu katika hatua za kibinadamu- Mtaalam wa UM

Tusipoteze fursa ya kujumuisha walemavu katika hatua za kibinadamu- Mtaalam wa UM

Siku chache kabla kuanza mkutano kuhusu Masuala ya Kibinadamu jijini Istanbul, Uturuki wiki ijayo, Mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wenye ulemavu, Catalina Devandas-Aguilar, ametoa wito kwa nchi zote duniani zizingatie haki za watu wenye ulemavu katika jitihada zao ka kibinadamu.

Mtaalam huyo wa haki za binadamu ametoa wito kwa serikali na mashirika yaunge mkono mkataba kuhusu kujumuisha watu wenye ulemavu katika jitihada za kibinadamu.

Mkataba huo, ambao ni fungu la kanuni za kufanya jitihada za kibinadamu kuwa jumuishi zaidi, utazinduliwa wakati wa kongamano hilo la Istanbul, la Mei 23 hadi 24, 2016.

Bi Devandas-Aguilar amesema mkutano huo wa masuala ya kibinadamu ni fursa ya aina yake ya kuimarisha uungaji mkono wa kimataifa kuhusu ujumuishaji wa watu wenye ulemavu katika jitihada zote za kibinadamu, ikiwemo uhamasishaji, uvumbuzi, uwekaji viwango wastani, na ushiriki wa mashirika ya kiraia na ushirikiano wa kimataifa.