Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zeid apongeza Pfizer kukataa dawa zake kutumika kwenye mauaji

Zeid apongeza Pfizer kukataa dawa zake kutumika kwenye mauaji

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein amekaribisha uamuzi wa kampuni ya dawa duniani, Pfizer ya kutaka dawa zake zisitumike kwenye mauaji kupitia sindano za sumu.

Amenukuliwa katika taarifa akisema kuwa wafanyabiashara kwenye sekta mbali mbali wanaweza kusaidia kuzuia ukiukwaji wa haki za binadamu na inatia moyo kuona kampuni zinashiriki vyema kutokomeza adhabu ya kifo.

Pfizer ilitangaza itadhibiti mauzo ya aina saba ya dawa ambazo zimekuwa zikitumika kwenye sindano za kifo kwenye baadhi ya nchi na kwamba zitauzwa kwa serikali chini ya uthibitisho kuwa hazitatumika kutekeleza adhabu za kijinai.

Zeid ametoa wito kwa sekta ya biashara kuzingatia wajibu wa kibinadamu kama ilivyobainishwa kwenye kanuni ongozi za Umoja wa Mataifa kuhusu biashara na haki za binadamu.