Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usaidizi kwa wakimbizi wapaswa kulenga zaidi walio mjini: Eliasson

Usaidizi kwa wakimbizi wapaswa kulenga zaidi walio mjini: Eliasson

Zaidi ya nusu ya wakimbizi duniani kote hawaishi kwenye kambi za wakimbizi, bali kwenye miji, na mara nyingi kwenye makazi duni wakikosa huduma za msingi za elimu, afya na ajira.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson amesema hayo akihutubia mkutano uliofanyika leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuhusu njia bora na bunifu za kukabiliana na suala hilo.

Bwana Eliasson ameeleza kwamba usaidizi wa mashirika ya kibinadamu hulenga zaidi wakimbizi waliopo kambini na kusahau wanaoishi mijini, akisema:

(Sauti ya Bwana Eliasson)

“Mara nyingi wanaishia kwenye makazi duni au yasiyokuwa rasmi pembezoni mwa miji, kwenye maeneo yaliyojaa na yenye hatari za mafuriko, majanga ya afya na magonjwa.”

Hata hivyo amesema tangu mwaka 2009, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi UNHCR limejitahidi kubadilisha mikakati yake na kulenga zaidi wakimbizi wanaoishi mijini.

Hatimaye amesisitiza kwamba kupokea wakimbizi pia inaweza kuwa fursa kwa uchumi wa nchi.

(Sauti ya Bwana Eliasson)

“Kwenye nchi nyingi duniani, wakimbizi mara nyingi wanachukua kazi zenye mishahara midogo na wanatoa huduma kwenye sekta kama kazi za nyumbani na shambani. “

Mkutano huo ni moja ya hatua ya kuelekea mkutano wa kimataifa kuhusu suala la wakimbizi na wahamiaji utakaofanyika mjini New York, Marekani tarehe 19 Septemba mwaka huu.