Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shule nne au hospitali zinashambuliwa au kukaliwa kila siku:UNICEF

Shule nne au hospitali zinashambuliwa au kukaliwa kila siku:UNICEF

Wastani wa shule nne au hospitali zinashambuliwa au kuchukuliwa na makundi au vmajeshi yenye silaha kila siku. Hii ni kwa mujibu wa uchambuzi shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia watoto UNICEF uliotolewa kabla ya mkutano wa dunia wa masuala ya kibinadamu.

Matokeo ya utafiti yaliyotolewa na ripoti ya karibuni ya mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa kuhusu watoto na migogoro ya silaha , imekuja wakati kumekuwa na mashambulio ya karibuni katika majengo ya elimu, afya na dhidi ya wafanyakazi, ikiwa ni pamoja na mambomu kwenye shule nchini Yemen na hospitali mjini Aleppo Syria ambapo watu takribani 50 waliuawa akiwemo Daktari wa miwsho aliosalia wa watoto.

Afshan Khan mkurugenzi wa UNICEF wa mpango wa dharura anasema watoto wanauawa, kujeruhiwa na kupewa vilema vya maisha katika maeneo ambayo wanapaswa kulindwa.

Ameongeza kuwa mashambulizi dhidi ya shule na hospital ni miongoni mwa aina sita za ukiukaji dhidi ya watoto ulioorodheshwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. Ripoti ya mwisho ya Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa kuhusu watoto na migogoro ya silaha imeorodhesha visa zaidi ya 1500 vya mashambulizi au matumizi ya kijeshi ya shule na hospitali mwaka 2014 ikiwemo nchini Afghanistan, Syria, Yemen, Sudan Kusini na Nigeria.