Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wajumbe wa Baraza la Usalama wawasili Kenya

Wajumbe wa Baraza la Usalama wawasili Kenya

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamewasili mjini Nairobi, Kenya ambapo kesho watakwenda Somalia katika ziara yao kwenye nchi hiyo iliyoko pembe ya Afrika.

Akizungumza baada ya kuwasili mjini Nairobi, Rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Mei Balozi Amr Abdellatif Aboulatta wa Misri amesema miongoni mwa ajenda muhimu ni mazungumzo na Rais wa Somalia na wadau wengine kuhusu uchaguzi nchini humo mwezi Agosti mwaka huu akisema..

(Sauti ya Balozi Aboulatta-1)

“Tuko hapa kuona iwapo Somalia watafanya uchaguzi kama ilivyopangwa au la. Somalia ni muhimu sana katika pembe ya Afrika. Pia ni muhimu kukutana na viongozi wa Kenya, Ijumaa tutakutana na Rais tunatumai atatushauri kuhusu vile anavyoona hali ilivyo pembe ya Afrika, hususan Somalia.”

Balozi Aboullata ambaye pia ni mwakilishi wa kudumu wa Misri kwenye Umoja wa Mataifa akaulizwa iwapo hali ya Somalia inatia matumaini..

(Sauti ya Balozi Aboulatta-2)

“Hali inazidi kuwa bora na ndio maana tuko hapa kuwatia moyo na kuleta ujumbe wa Baraza la Usalama kuwaunga mkono, na kuwashinikiza wafanye uchaguzi muda waliopanga ili tuweze kusonga mbele na mipango ya kuimarisha utulivu Somalia ambayo ni muhimu kwa pembe ya Afrika.”

Baada ya Somalia na kuzungumza na waandishi wa habari baaadaye mjini Nairobi, wajumbe wa Baraza la Usalama wataelekea Cairo, Misri.