Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban azungumza na Rais Kenyatta kwa simu kuhusu Dadaab

Ban azungumza na Rais Kenyatta kwa simu kuhusu Dadaab

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amefanya mazungumzo leo kwa njia ya simu na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, kufuatia uamuzi uliochukuliwa na serikali ya Kenya mnamo tarehe 6 Mei 2016 kufunga kambi ya wakimbizi ya Dadaab.

Ban ameeleza shukrani zake kwa Rais Kenyatta na watu wa Kenya, kwa ukarimu wao wa miongo mingi kwa idadi kubwa ya waomba hifadhi na wakimbizi.

Katibu Mkuu amemhakikishia Rais Kenyatta kwamba anatambua jukumu na wajibu mkubwa unaoambatana na kuwapa hifadhi wakimbizi wengi, katika mazingira ya changamoto za kiusalama.

Aidha, Ban ametoa wito kwa Rais Kenyatta aendelee kutumia makubaliano ya pande tatu yaliyosainiwa mnamo Novemba 2013, baina ya serikali ya Kenya, serikali ya Somalia, na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kama msingi wa wakimbizi wa Somalia kurejea makwao kwa hiari yao, kwa usalama na kwa utu.

Katika mazungumzo hayo, Ban ametaja kuwa Naibu Katibu Mkuu, Jan Eliasson na Kamishna Mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi, watafanya ziara nchini Kenya mwishoni mwa mwezi Mei, 2016, ili kujadili kuhusu suala hilo, na kusisitiza utayari wa Umoja wa Mataifa kuchagiza jamii ya kimataifa kuinga mkono Kenya katika kukabiliana na changamoto za wakimbizi.