Skip to main content

Dola Milioni 110 kukwamua nchi zenye ukame Afrika- IFRC

Dola Milioni 110 kukwamua nchi zenye ukame Afrika- IFRC

Shirikisho la Msalaba Mwekundu na Hilal Nyekundu, IFRC limeahidi dola Milioni 110 kusaidia miradi ya kukwamua nchi zilizokumbwa na ukame kusini mwa Afrika.

Miradi hiyo kama vile mgao wa chakula, mafunzo ya mbinu za umwagiliaji na kilimo bora inalenga watu Milioni Moja katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Nchi husika, Afrika Kusini, Lesotho, Malawi, Msumbiji, Namibia na Zimbabwe zilishuhudia kiwango kidogo cha mvua mwaka 2015, na kama haitoshi ukame uliochochewa na El Nino umechelewesha upanzi na kuathiri mazao.

Takwimu zinaonyesha kuwa Afrika Kusini pekee inatarajiwa kushuhudia kuporomoka kwa asilimia 18 ya mavuno ya ngano kwa msimu wa baridi na hivyo italazimika kuagiza kutoka nje asilimia 60 ya mahitaji ya ngano.

IFRC imesema katika hali hiyo watu wapatao Milioni 31 na Nusu kwenye eneo hilo wanahaha kusaka mlo bora na idadi hiyo inatarajiwa kufikia Milioni 49 mwishoni mwa mwaka huu.