Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Virusi vya Zika huenda vikatua Ulaya hivi karibuni- WHO

Virusi vya Zika huenda vikatua Ulaya hivi karibuni- WHO

Shirika la Afya Duniani (WHO), limesema kuwa bara la Ulaya linakabiliwa na hatari ya kukumbwa na mlipuko wa virusi vya Zika katika majira ya joto, ingawa hatari hiyo inakadiriwa kuwa kwa kiwango kidogo hadi cha wastani. John Kibego na taarifa zaidi.

(TAARIFA YA KIBEGO)

Kulingana na tathmini mpya iliyochapishwa na Ofisi ya WHO barani Ulaya, ingawa hatari hiyo ya mlipuko wa Zika inatofautiana katika maeneo mbalimbali barani Ulaya, kiwango chake ni kikubwa zaidi katika nchi zilizo na mbu aina ya Aedes, ambaye husambaza virusi hivyo.

WHO imetoa wito hususan kwa nchi zinazokabiliwa na hatari kubwa zaidi kuimarisha uwezo wao kitaifa, na kuweka kipaumbele hatua zitakazozuia mlipuko mkubwa wa Zika.

Mkurugenzi wa WHO kanda ya Ulaya, Zsuzsanna Jakab, amesema kufuatia tathmini hiyo ya hatari, WHO inataka kufahamisha na kulenga kazi ya kuchukua tahadhari katika kila nchi, kulingana na kiwango cha hatari.