Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa waisihi Urusi kuheshimu haki za watatar Crimea

Umoja wa Mataifa waisihi Urusi kuheshimu haki za watatar Crimea

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imeisihi Urusi kuhakikisha haki za watu wa asili na walio wachache zinaheshimiwa kwenye eneo la Crimea.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi, msemaji wa ofisi hiyo Rupert Colville amesema hali ya watu wa jamii ya Tatar ambao makazi yao ni Crimea inaendelea kutia wasiwasi, taasisi yao ya uwakilishi iitwayo Mejilis ikiwa imepigwa marufuku.

(Sauti ya Bwana Colville)

“ Tumetiwa wasiwasi sana na kile kinachoitwa mahakama kuu ya Crimea kupiga marufuku Mejilis. Tunahofia kwamba inayojidai kuwa “mahakama” kutambua Mejilis kama shirika lenye msimamo mkali kutawaacha watatar wa Crimea kwenye hatari kubwa zaidi ya ukiukwaji wa haki za binadamu na adhabu za pamoja.”

Aidha bwana Colville amesema ripoti zinaonyesha kuwa watu wa jamii ya Tatar wanazidi kunyanyaswa na kuteswa Crimea.

Wito huo umetolewa wakati ambapo miaka 72 iliyopita, mnamo tarehe 18 Mei 1944, watatar 200,000 walifurushwa makwao na serikali ya Muungano wa Jamhuri za Kisovieti za Kisoshalisti (USSR), wengi wao wakifariki dunia kwenye safari ya kuwapeleka kwa nguvu nchini Uzbekistan.