Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Visa 44 vya unyanyasaji wa kingono vimeripotiwa 2016 katika ulinzi amani- UM

Visa 44 vya unyanyasaji wa kingono vimeripotiwa 2016 katika ulinzi amani- UM

Idadi ya visa vya unyanyasaji wa kingono unaodaiwa kufanywa katika operesheni za Umoja wa Mataifa za ulinzi wa amani na ujumbe maalum wa kisiasa mwaka 2016 vimefikia 44.

Hayo yametangazwa leo na Msemaji wa Katibu Mkuu, Stephane Dujarric, akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani.

Bwana Dujarric amesema kati ya visa hivyo 44, visa 29 vimeripotiwa katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati MINUSCA), saba katika ujumbe wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO), na viwili katika ujumbe wa Haiti (MINUSTAH). Aidha, kumeripotiwa kisa kimoja katika kila moja ya ujumbe ufuatao: UNMISS, Sudan Kusini, UNOCI katika Côte d’Ivoire, MINUSMA, nchini Mali, UNIFSA eneo la Abyei, UNSMIL nchini Libya, na kimoja katika ujumbe wa kuratatibu mchakato wa amani Mashariki ya Kati, UNSCO.

Amesema visa 39 kati ya vyote 44 vinahusu wafanyakazi wa vikosi vya usalama, huku akitangaza kinachofanywa na Umoja wa Mataifa kukabiliana na tatizo hilo.

“Pia tuna taarifa zaidi kuhusu kinachofanywa katika mikakati muhimu, ikiwemo kufanyia ukaguzi watu wote wanaopelekwa katika ujumbe ili kuona iwapo wamewahi kushiriki vitendo vinavyokiuka maadili, na kuweka timu za kukabiliana na visa hivyo mara moja, kukusanya taarifa za ushahidi pale madai ya unyanyasaji wa kingono yanapoibuka.”

Aidha amezungumzia mfuko wa fedha kwa waathirika wa unyanyasaji..

“Na kama mjuavyo, tulizindua mfuko wa fedha kuwasaidia waathirika wa vitendo hivyo mwezi machi. Tayari Norway imechangia dola 125,000, na tunahimiza nchi zingine wachama wachangie pia.”