Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari na mawasiliano ni muhimu katika ajenda ya 2030:Ban

Habari na mawasiliano ni muhimu katika ajenda ya 2030:Ban

Jumuiya ya kimataifa sasa inahamasishwa ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu, ambayo inatambua uwezo mkubwa wa habari na teknolojia ya mawasiliano (ICT) ili kuharakisha maendeleo ya binadamu, kuziba pengo la kidijitali na kuongeza maarifa.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon katika ujumbe maalumu wa siku ya kimataifa ya habari na mawasiliano ambayo huadhimishwa Mei 17. Ameongeza kuwa malengo 17 ya maendeleo endelevu yanataka kujumuishwa teknolojia ya habari na mawasiliano , ili kun’gamua mtazamo wa jumla wa utu kwa maisha ya watu wote.

Amesema teknolojia hizi zinatoa suluhu za kushughulikia matatizo ya mabadiliko ya tabia nchi, njaa, umasikini na changamoto zingine za kimataifa.Pia ni za muhimu katika kutoa huduma za afya , fursa za elimu, kuwawesesha wanawake, kuongeza ufanisi viwandani, katika sekta ya kilimo na kulinda mazingira.

Ametoa wito kwa serikali, sekta ya biashara na viongozi wa asasi za kiraia kuendeleza teknolojia mpya ambazo zina mafanikio ya kudumu kwa jamii. ICT inaweza kujenga jamii jumuishi na watu wenye ulemavu.