Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwenye Siku ya Familia, Ban asihi serikali zisaidie familia kujikimu kimaisha

Kwenye Siku ya Familia, Ban asihi serikali zisaidie familia kujikimu kimaisha

Ikiwa leo Mei 15 ni Siku ya Kimataifa ya Familia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametoa wito kwa serikali zitambue na kuunga mkono mchango muhimu wa familia katika nyanja mbalimbali za maisha.

Katibu Mkuu amesema maadhimisho ya siku ya familia mwaka huu yanakuja wakati wa misukosuko na majanga kwa familia kote duniani, kutokana na kuenea kwa itikadi kali katili, vita na watu kulazimika kuhama makwao, majanga ya hali ya hewa, na changamoto zingine zinazoathiri afya na ustawi wa familia katika hali hizo za mizozo.

Akimulika hasa watoto, vijana, wanawake na wazee, Ban amesema watoto hunawiri zaidi wanapoonyeshwa upendo na kupata huduma za afya, elimu, na vitu vingine vya msingi.

Amesema wanawake katika jamii nyingi hubaguliwa na kukumbana na ukatili katika familia zao, ambao huwa na madhara makubwa kwa afya na maisha yao kwa ujumla.

Kuhusu wazee, Ban amesema maisha ya familia ni muhimu kwa afya ya wazee, ambao huwa na afya njema pale mchango wao katika familia na jamii unapotambuliwa.

Katika ujumbe wake, Katibu Mkuu pia amemulika vijana barubaru, akisema wanahitaji usaidizi wa kisaikolojia na ushauri nasaha, akitaja visa vya kujiua hasa miongoni mwa vijana wanaojikuta katika mapenzi ya jinsia moja au wenye jinsia tofauti na maumbile.

Kwa ujumla, Ban amesema familia ziko mstari wa mbele katika juhudi za kimataifa za kutimiza ajenda kabambe ya 2030 kuhusu maendeleo endelevu, hususan lengo la SDG3, ambalo linahusu kuendeleza maisha yenye afya na maisha bora kwa watu wenye umri mbalimbali.