Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asifu hatua za mapambano dhidi ya Boko Haram, ahofia haki za binadamu

Ban asifu hatua za mapambano dhidi ya Boko Haram, ahofia haki za binadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amekaribisha hatua za pamoja zilizopigwa na nchi za Afrika Magharibi katika kupambana na magaidi wa Boko Haram, na kusifu dhamira ya nchi hizo ya kufanya operesheni za paomja, lakini akaeleza kusikitishwa na ripoti za ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu wakati wa operesheni hizo.

Ban amesema hayo katika ujumbe wake kwa mkutano wa pili wa ukanda wa Afrika Magharibi kuhusu usalama, ambao umehudhuriwa na Rais wa Nigeria Mummadu Buhari na Rais wa Ufaransa, François Hollande.

Katika ujumbe uliosomwa na Mwakilishi wake maalum na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa Afrika ya Magharibi, Mohamed Ibn Chambas, Ban amesema tangu kuanza kwa mzozo wa Boko Haram, takriban watu milioni 2.8 wamelazimika kuhama makwao ndani ya nchi, huku wengine 500,000 wakikimbilia nchi jirani kutafuta usalama.

Aidha, Katibu Mkuu amepongeza ukarimu wa nchi jirani, na kukaribisha taarifa kuwa serikali za ukanda huo na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, zitaanza mazungumzo kuhusu kurejea kwa hiari nyumbani kwa wakimbizi hao.