Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa umeshapiga hatua dhidi ya uhalifu wa kingono

Umoja wa Mataifa umeshapiga hatua dhidi ya uhalifu wa kingono

Umoja wa Mataifa umeshapiga hatua kubwa katika kupambana na ukatili wa kingono unaofanywa na walinda amani wa Umoja huo, wamesema leo wataalam walioshiriki kwenye mjadala uliofanyika mjini New York kuhusu suala hilo.

Akihutubia mjadala huo, Jane Holl Lute, ambaye ni Mratibu Maalum wa kuimarisha jitihada za Umoja wa Mataifa kuhusu suala hilo, ameeleza kwamba mitazamo ya uongozi katika ujumbe wa ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa duniani kote imeshabadilika na kusababisha wadau wote kuheshimu zaidi kanuni za Umoja huo:

(Sauti ya Bi Lute)

“Tunataka kujulikana kama mfumo unaoheshimu kanuni, na kanuni zetu zinapaswa kuwa wazi. Tunapaswa kuweka wazi kanuni zetu ni nini na tumeshapata mafanikio mengi katika hilo.”

Amezungumzia alichoshuhudia kwenye ziara yake nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, ambapo makamanda wameimarisha harakati za kuzuia uhalifu wa kijinsia.

Kwa upande wake Atul Khare, ambaye ni msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa masuala ya operesheni mashinani, amesema tayari Umoja wa Mataifa umeunda mfuko wa kusaidia wahanga wa uhalifu wa kingono na watoto wanaozaliwa kutokana na uhalifu huo, akizisihi nchi wanachama kufadhili mfuko huo.

Aidha amesema ni wajibu wa nchi wanachama kupeleka mbele ya sheria walinda amani wanaoshukiwa kutekeleza uhalifu huo, akipongeza Misri, Bangladesh na Afrika Kusini kwa kuchukua hatua za kisheria haraka dhidi ya wahalifu.