Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalam wa UM wataka hatua haraka kuhusu Mkataba wa Paris

Wataalam wa UM wataka hatua haraka kuhusu Mkataba wa Paris

Wataalam wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa, wamesema kuwa ingawa Mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi ndio wa kwanza unaojumuisha ulinzi wa haki za binadamu katika suala la mazingira, nchi wanachama zinakabiliwa na mtihani mkubwa wa kuweka dhamira zao katika vitendo.

John H. Knox, ambaye ni mtaalam maalum kuhusu haki za binadamu na mazingira, amesema mtihani wa kwanza utakuwa wiki ijayo, wakati wawakilishi wa serikali watakutana jijini Bonn, Ujerumani.

Wawakilishi hao wanatarajiwa kujadili kanuni za mkakati mpya wa kimataifa wa kuhamisha fedha kutoka nchi zilizoendelea na kuzipeleka nchi zinazoendelea kwa minajili ya kusaidia miradi itakayochangia katika kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi na kusaidia juhudi za maendeleo endelevu.

Bwana Knox amesema, inatia moyo kuona kwamba tayari nchi 177 zimetia saini mkataba huo katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja, lakini kazi ngumu ya kutunza mazingira na haki za binadamu ndiyo sasa inaanza.