Skip to main content

Kilimo ni uti wa mgongo wa maendeleo Afrika: WEF Kigali

Kilimo ni uti wa mgongo wa maendeleo Afrika: WEF Kigali

Mamilioni ya watu wanaweza kujikwamua na umaskini barani Afrika, iwapo bara hilo litawekeza zaidi katika sekta ya kilimo, amesema leo Kanayo Nwanze, Rais wa Mfuko wa Kimataifa kwa Maendeleo ya Kilimo IFAD, akisisitiza kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa maendeleo barani humo.

Bwana Nwanze ameyasema hayo leo akiongoza mazungumzo kuhusu kilimo endelevu na mabadiliko ya tabianchi barani Afrika kwenye mjadala wa kimataifa wa kiuchumi, WEF unaoendelea wiki hii mjini Kigali, Rwanda.

Licha ya changamoto za kiuchumi, kiusalama na mabadilioko ya tabianchi zinazoikumba bara hilo, Bwana Nwanze amesema bado fursa kubwa za kiuchumi zipo huku ongezeko la idadi ya watu na ukuaji wa tabaka la kati zikisababisha kuongezeka kwa mahitaji ya chakula.

Bwana Nwanze ameshangazwa na kuona kwamba bado Afrika inaingiza vyakula kutoka nje wakati ikiwa na uwezo wa kujitegema.

(Sauti ya Nwanze)

“Bara letu linaendelea kutumia dola bilioni 35 kila mwaka kuingiza vyakula. Takwimu zetu za hivi karibuni zinaonyesha kwamba tunazalisha asilimia 130 za mahitaji yetu ya chakula. Nadhani ni ujinga kabisa kwamba bara tajiri kama Afrika linatumia dola bilioni 35 kuzalisha ajira mahali pengine.”