Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yazindua miongozo kuhusu matumizi ya dawa za kuulia wadudu

FAO yazindua miongozo kuhusu matumizi ya dawa za kuulia wadudu

Dawa za kuulia wadudu zinaweza kusababisha madhara makubwa kwa afya ya binadamu na mazingira, ambayo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula FAO, kwa ushirikiano na Shirika la Afya Duniani WHO limejaribu kuzidhibiti kupitia miongozo mipya iliyotolewa leo.

Kwa mujibu wa taarifa ya FAO, nchi zinazoendelea ziko hatarini zaidi kukumbwa na madhara yatokanayo na matumizi ya dawa hizo, kwani wakulima wadogo wadogo mara nyingi hawana vifaa vya kujikinga wakipulizia dawa shambani, huku wakitumia aina za dawa zenye hatari kubwa zaidi ambazo zimeshakatazwa kwenye nchi zilizoendelea.

Madhara ya dawa hizo ni visa vya kuathirika na sumu zake moja kwa moja, kuugua saratani, kuathiri ukuaji wa watoto, na kuharibu mazingira.

FAO imesema suluhu ni kutumia dawa zisizo na hatari kubwa, na vilevile kupendelea njia mbadala na endelevu za kudhibiti uwepo wa wadudu.

Miongozo ya FAO itasaidia serikali kuchukua hatua mbalimbali ili kutathmini hatari zilizopo na kuzidhibiti pamoja na kukuza matumizi ya njia mbadala za kudhibiti wadudu.