Skip to main content

Jan Eliasson akumbusha nchi wanachama majukumu yao katika amani ya kimataifa

Jan Eliasson akumbusha nchi wanachama majukumu yao katika amani ya kimataifa

Asilimia 80 ya mahitaji ya kibinadamu duniani kote yamesababishwa na mizozo na vita, amekumbusha leo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson.

Amesema hayo akihutubia mkutano wa ngazi ya juu kuhusu hatari dhidi ya amani na usalama wa kimataifa, ambao umefanyika leo kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Ameeleza kwamba mizozo ya kisasa inaupa Umoja wa Mataifa changamoto nyingi, na ni lazima mfumo huo ubadilike ili uwe na ufanisi zaidi.

Sanjari na hiyo, amesisitiza umuhimu wa kuzuia mizozo kama msingi wa kazi ya Umoja wa Mataifa, kupendelea suluhu jumuishi za kisiasa, pamoja na kutegemea ubia bora wa kimataifa.

Akimulika jitihada zilizotekelezwa na Umoja wa Mataifa, ikiwemo mapambano dhidi ya uhalifu wa kijinsia unaofanywa na walinda amani, amemulika majukumu ya nchi wanachama katika kuzuia mizozo.

(Sauti ya Bwana Eliasson)

“Jinsi mnavyoona, mfumo wa Umoja wa Mataifa umejituma kutekeleza ajenda hiyo ya mabadiliko. Lakini hatuwezi kuitimiza pekee yetu. Kazi hiyo inahitaji dhamira ya pamoja ya Umoja wa Mataifa na nchi wanachama. Lakini kwenye baadhi ya maeneo, dhamira za balagha hazijageuka hatua thabiti.”