Mchango mzuri wa wahamiaji na wakimbizi wapaswa kuzingatiwa: Eliasson

Mchango mzuri wa wahamiaji na wakimbizi wapaswa kuzingatiwa: Eliasson

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson amezingatia mchango mzuri wa wahamiaji na wakimbizi kwenye jamii, akiwasilisha leo ripoti mpya ya Katibu Mkuu kuhusu jinsi ya kukabiliana kwa usalama na idadi kubwa ya wahamiaji na wakimbizi duniani kote.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Bwana Eliasson amekumbusha kwamba wahamiaji na wakimbizi wanakumbwa na mateso mengi, kwenye nchi zao, safarini na wanapowasili kwenye nchi wanakotafuta hifadhi.

Amesikitika kuhusu mtazamo mbaya unaoenea kuhusu suala hilo.

(Sauti ya Bwana Eliasson)

“ Unaona mijadala kuhusu wahamiaji na wakimbizi inatenganisha nchi na mijadala ya kisiasa, inagawanya mtazamo wa jamii na vyama vya kisiasa. Imekuwa sasa eneo ambapo nadhani ni muhimu kwa sisi kama muundo kujikumbusha kuhusu maana ya uhamiaji.”

Kuhusu mchango mzuri wa uhamiaji, ametaja ukuaji wa uchumi, ongezeko la idadi ya watu linalosaidia Marekani na Ulaya kutopungukiwa kwa watu, na mchango wa pesa zinazotumwa na wahamiaji kwenye nchi zinazoendelea ambao ni mara tatu kiasi cha pesa kinachotumwa kupitia usaidizi wa kimataifa.

Hatimaye amesisitiza kwamba utofauti wa kitamaduni kwenye jamii pia ni kitu kizuri, akisikitikia kuhusu ongezeko la ubaguzi duniani kote dhidi ya wakimbizi .

Kwa mujibu wa ripoti hii kuhusu utu na usalama kwa wahamiaji na wakimbizi, idadi ya wakimbizi wa ndani ni milioni 40, wakimbizi wenyewe ni milioni 20, huku idadi ya wahamiaji ikiwa ni takriban milioni 240.

Miongoni mwa mapendekezo ya ripoti hii ni kuimarisha usalama wa wahamiaji, hasa kwa kupambana na biashara haramu ya wahamiaji, kugawana majukumu katika kupokea wakimbizi baina ya nchi mzozo unapoibuka kwenye nchi, na kuimiarisha ushirikiano baina ya mashirika ya kimataifa yanayohusiana na suala hilo.

Mapendekezo hayo yatazungumzwa tarehe 19 Septemba mwaka huu kwenye mkutano wa ngazi ya juu itakayofanyika mjini New York kuhusu suala hilo siku moja tu kabla ya kikao chaa 71 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.