Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OCHA yaomboleza kifo cha mhudumu wa kibinadamu DRC

OCHA yaomboleza kifo cha mhudumu wa kibinadamu DRC

Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) na wadau wa kibinadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), wanaomboleza kifo cha mhudumu wa kibinadamu, wakili Roger Muteba Muanyishayi.

Wakili huyo alifariki dunia mnamo Mei 6, wakati gari la shirika lisilo la kibinadamu alimokuwa akisafiria lilipojikuta katikati ya mapigano, eneo la Masisi, jimbo la Kivu Kaskazini.

Taarifa ya OCHA imesema kifo cha wakili huyo hakipaswi kunyamaziwa, kwani ni dhihirisho la hali mbaya ya usalama ambayo inaathiri maisha ya watu wengi nchini DRC.

Halikadhalika, OCHA imesema kifo hicho ni ukumbusho wa hatari wanazokumbana nazo wahudumu wa kibinadamu wanapotoa huduma za kunusuru maisha, na haja ya wenye mamlaka kuhakikisha usalama wao.