Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban aipongeza Ushelisheli kwa vita dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi:

Ban aipongeza Ushelisheli kwa vita dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi:

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameipongeza serikali ya Ushelisheli kwa kuwa miongoni mwa nchi 16 za kwanza kuruidhia mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.

Baada ya mazungumzo yake na Rais James Alix Michel na baraza la mawaziri , Ban akizungumza na waandishi wa habari  amesema, ana imani Ushelisheli itaendeleza rekodi yake kama nguzo imara ya demokrasia.

Kisiwa hicho ambacho kimebarikiwa na mali asili amekipongeza pia kwa uhifadhi wa mazingira baada ya kuzuru eneo la urithi wa dunia, lakini pia mchango wake katika kukabiliana na changamoto kubwa zinazoikabili dunia zikiwemo umasikini, mabadiliko ya tabia nchi na usalama mdogo.

(SAUTI YA BAN)

"Ziara yangu Ushelisheli imetimiza hisia yangu kuwa mataifa ya visiwa vidogo wametambua sauti zao na wako tayari kuongoza. Mna jukumu muhimu kuwa mstari wa mbele katika mabadiliko ya tabia nchi kutukumbusha sote kuhusu mwingiliano wa dunia yetu na nini tutapoteza kama hatuweza kuchukua hatua sasa.”

Ban ameishukuru pia Ushelisheli kwa vita dhidi ya uharamia kwenye pwani ya Somalia, kudumisha haki za binadamu na kushirikiana na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Madawa na uhalifu UNODC kuhakikisha kwamba washukiwa wanapewa haki zinazostahili katika kesi zao.

Kesho Ban atazuru kituo cha walinzi wa pwani ambako atasikia mitazamo ya kukabiliana na uhalifu baharini.

Taifa hilo ambalo liko katika hatari ya vimbunga kikiwepo cha karibuni cha Fantala, Ban amesema ana tumai litaelezea uzoefu wake kwenye mkutano wa kimataifa wa masuala ya kibinadamu utakaofanyika Istanbull Uturuki Mai 23 na 24.