Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kubiš asihi umoja Iraq ili kuondoa mkwamo wa kisiasa

Kubiš asihi umoja Iraq ili kuondoa mkwamo wa kisiasa

Tangu nihutubie baraza hili, mzozo mkubwa wa kisiasa umekumba Iraq na kusababisha mdororo na mkwamo wa utendaji wa serikali na baraza la wawakilishi.

Hiyo ni kauli ya Ján Kubiš, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, alipoanza kuhutubia Baraza la Usalama hii leo kuhusu hali ilivyo nchini Iraq na utekelezaji wa majukumu ya ofisi anayoongoza, UNAMI.

Amesema mkwamo huo umeleta hali mbaya zaidi kwenye nchi ambayo tayari inakabiliwa na changamoto za kijeshi, kiusalama, kiuchumi na kibinadamu, hivyo akatoa rai.

(Sauti ya Kubiš)

“Natoa rai ya dhati kwa viongozi wa kiserikali, kisiasa na kiraia kushirikiana kupitia mashauriano yenye lengo la siyo tu kumaliza mkwamo wa kisiasa bali pia kutoa mwelekeo dhahiri wa mustakhbali wa wananchi wa Iraq bila kujali dini au kabila, mwelekeo ambao utawaunganisha na viongozi ndani ya Iraq iliyo moja.”

Amesema utulivu, usalama na umoja nchini Iraq vinategemea mfumo wa kisiasa ambao ni thabiti na shirikishi na ambao unazingatia usawa kwenye utoaji uamuzi katika ngazi ya serikali kuu na mitaa, sambamba na suluhu bora zinazoepusha watu kuenguliwa kisiasa au kidini.