Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zeid alaani shambulio dhidi ya wakimbizi wa ndani Syria

Zeid alaani shambulio dhidi ya wakimbizi wa ndani Syria

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu Zeid Ra’ad al Hussein amelaani vikali mashambulizi yaliyotokea alhamis dhidi ya kambi mbili za wakimbizi wa ndani kaskazini magharibi mwa Syria, ambako watu wapatao 30 wameuawa, wakiwemo watoto.

Bwana Zeid amesema kwamba kambi hizo zimekuwepo pale kwa kipindi cha wiki kadhaa na kuonekana vizuri kutoka angani kwa hiyo ni dhahiri kuwa zimelengwa makusudi na washambuliaji, huo ni uhalifu wa kivita. Kwanye taarifa iliyotolewa na ofisi yake leo, Kamishna Zeid amesema kwamba yeye na ofisi yake watafanya bidii zote ili kubaini watekelezaji wa uhalifu huo aliouita wa kuleta hizaya.

Wengi wa wakimbizi wa ndani zaidi ya 2,500 waliotafuta hifadhi kwenye kambi hizo walikuwa ni wakazi wa Aleppo waliokimbia mashambulizi ya makombora mjini humo mwezi Februari mwaka huu.

Kamishna Zeid amesikitikia janga linalowakumba Wasyria: baada ya kushambuliwa nyumbani, wanashambuliwa kambini, wanazuiliwa kutafuta hifadhi kwenye nchi jirani, wako hatarini kupoteza maisha katika safari ya kuelekea Ulaya ambako hatimaye wanakumbwa na ubaguzi.

Hatimaye ametoa wito kwa nchi wanachama wa Baraza la Usalama, akiziomba kukubalia kupeleka kesi ya Syria mbele ya Baraza la Usalama.