Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuzuia ukatili wa kingono kuambatane na uwajibishaji kwa uhalifu

Kuzuia ukatili wa kingono kuambatane na uwajibishaji kwa uhalifu

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili wa kingono katika vita, Zainab Hawa Bangura, amewasili mjini Juba, Sudan Kusini leo Alhamis ya tahere 5 Mei, ambapo amesema kuwa kuzuia visa vya ukatili wa kingono kunapaswa kwenda sanjari na uwajibikaji kwa uhalifu wa zamani.

Bi Bangura ambaye yupo nchini humo kwa ziara ya siku nne, amesema kwamba kujenga mifumo yenye misingi ya kitaaluma na uwajibikaji ni muhimu katika kushughulikia masuala ya ukatili wa kongono na ukiukaji wa haki za binadamu.

Amesema mikakati inapaswa kuwekwa ya kuhakikisha kuwa visa vya ubakaji, utekaji na aina nyingine za unyanyasaji havifanyiki.

“Kwa hiyo unaweza kukabiliana na uwajibikaji kwa uhalifu wa zamani, lakini kilicho muhimu zaidi ni jinsi unavyosaidia serikali kuweka mikakati ndani ya serikali ya kuhakikisha kwamba kitu hiki hakitokei tena, kwa hiyo kwangu mimi hilo ni la kipaumbele. Kuanzia sasa ni kuhakikisha kuwa kinakomeshwa na hakifanyiki tena. Ndiyo maana tunafanya kazi na jeshi la SPLA kuunda mifumo katika jeshi ambapo wanajeshi wenyewe watajiwajibisha na kuwashitaki wenzao, na kuzuia ubakaji kufanyika tena.”