UM unaunga mkono Bosnia na Herzegovina kujiunga na EU, licha ya sintofahamu
Mwanamke wakiislamu wa Bosnia akingoja pamoja na watoto wake katika eneo la ukaguzi linalosimamiwa na polisi wa Bosnia na Croatia. [Mei 1994].
Picha: UN Picha / John Isaac[/caption]Mwakilishi mwandamizi wa Katibu Mkuu kuhusu Bosnia na Herzegovina, Valentin Inzko, amesema Umoja wa Mataifa unaunga mkono kwa dhati taifa hilo katika matamanio yake ya kujiunga na Muungano wa Ulaya (EU), kwa kuzingatia kwamba mabadiliko yanayotakiwa kufanywa kabla ya kufikia hatua hiyo yatakuwa yenye manufaa kwa raia wake.
Hata hivyo, amesema licha ya kuwasilisha ombi hilo mnamo Februari 15, 2016, taifa hilo linakabiliwa na kipindi chenye mtihani mkubwa, na kwamba linaweza kufaulu iwapo pande zote zitashirikiana na kuheshimu kikamilifu makubaliano ya amani ya Dayton.
Bwana Inzko amesema bado haijulikani dhahiri ni wakati gani inaweza kusemwa kuwa Bosnia na Herzegovina ipo kwenye mkondo mwema wa safari yake ya kujiunga na EU, lakini kuna la kutia moyo.
“Linalotia matumaini, kama nilivyosema, nchi hii iliwasilisha ombi la kujiunga na Muungano wa Ulaya. Sanjari na hili, mamlaka zake zimechukua hatua za kutekeleza ajenda ya mabadiliko, ikiwemo kuweka sheria mpya ya kazi kwa pande zote mbili. Ingawa tunakaribisha hatua zilizopigwa na mamlaka katika kufanya mabadiliko, tusiache kuwa makini kuhusu haja ya kuongeza kasi ya mabadiliko hayo. Lazima kuwe na kasi zaidi katika kufanya uamuzi.”