Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tugeuze Mkataba wa Paris kuwa vitendo sasa- Ban

Tugeuze Mkataba wa Paris kuwa vitendo sasa- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema hatua zinahitajika sasa, ili kuugeuza Mkataba wa Paris kuhusu tabianchi kuwa vitendo, kwa kuutekeleza haraka iwezekanavyo. Taarifa kamili na Flora Nducha..

Taarifa ya Flora

Ban amesema hayo jijini Washington D.C., Marekani, wakati wa mkutano wa kuchukua hatua kuhusu tabianchi mwaka 2016.

Katibu Mkuu amesema sasa ndio wakati wa kuongeza kasi na ukubwa wa hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, kwenye ngazi za kitaifa na kimataifa, kwa lengo la kubadilisha uchumi wa dunia ili kuwa na ulimwengu usiozalisha hewa ya ukaa katika nusu ya pili ya karne hii.

Mkutano huo unamulika maeneo matano ya ubia wa sekta mseto, ambayo ni nishati endelevu, matumizi endelevu ya ardhi, miji, usafiri, na nyenzo za kufanya uamuzi. Ban amesema vyote hivyo ni muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kutimiza malengo ya maendeleo endelevu.

“Kukabiliana na changamoto hizi, tunahitaji ubia imara kwa ngazi zote. Hakuna sekta ya jamii au nchi inayoweza kufaulu peke yake. Nawasihi mshirikiane. Mvumbue. Muwekeze. Pamoja, tunaweza kujenga ulimwengu tunaotaka, na ambao tutaona fahari kuuachia watoto wetu.”