Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutetea ubinadamu ndilo chaguo pekee, wasema waratibu wa UM

Kutetea ubinadamu ndilo chaguo pekee, wasema waratibu wa UM

Wiki chache kabla ya mkutano wa Istanbul kuhusu masuala ya kibinadamu, waratibu wa masuala ya kibinadamu Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, wamesema leo kuwa kutetea ubinadamu ndilo chaguo pekee lililopo sasa. Taarifa kamili na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Katika taarifa ya pamoja, waratibu hao ambao ni: Lise Grande/Iraq; Edward Kallon/Jordan; Philippe Lazzarini/Lebanon; Ali Al Za’atari/Libya; Robert Piper/Maeneo ya Wapalestina yaliyokaliwa; Yacoub El Hillo/ Syria; Kevin Kennedy/Mratibu wa Kikanda kuhusu mzozo wa Syria, na Jamie McGoldrick/Yemen, wamesema mamilioni ya watu Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini wanakumbana na taabu kubwa.

Wameongeza kwamba ghasia na ukatili ulioenea, pamoja na migogoro na itikadi kali Iraq, Libya, Palestina, Syria na Yemen, vinaongeza shinikizo la mahitaji ya kibinadamu na athari zinazovuka mipaka ya nchi hizo.

Watu milioni 55 katika ukanda mzima wanahitaji usaidizi wa kibinadamu kuhakikisha wanaendelea kuishi, wakiwa hawajui watatoa wapi mlo mwingine, na hawana huduma za afya, maji safi na kujisafi.