Suala la wakimbizi wa Palestina linanitia uchungu- Ban

Suala la wakimbizi wa Palestina linanitia uchungu- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameeleza kutiwa uchungu na suala la hatma ya wakimbizi wa Palestina wapatao milioni 5.2, ambalo halijapatiwa suluhu kwa muda mrefu.

Katibu Mkuu amesema hayo jijini New York wakati wa mkutano kuhusu kuimarisha usaidizi kwa wadhamini na wanaotoa hifadhi, kwa ajili ya uendelevu wa Shirika la Kuwasaidia Wakimbizi wa Palestina (UNRWA).

Ban amesema katika muktadha wa hali tete Mashariki ya Kati, wakimbizi wa Palestina wamo hatarini zaidi, kwani maeneo wanayoishi ama yameghubikwa na migogoro au yamo katika shinikizo la athari zitokanazo na migogoro maeneo jirani.

image
Pierre Krähenbühl, Kamishna Mkuu wa UNRWA akihutubia waandishi habari jijini New York mnamo tarehe 5 Machi 2016. Picha UM /Mark Garten
Katibu Mkuu amesema ni katika muktadha huu ndipo UNRWA na wafanyakazi wake 30,000 hutoa huduma muhimu za dharura na maendeleo ya binadamu kwa wakimbizi wa Palestina, akieleza umuhimu wa operesheni za UNRWA.

“Ni muhimu, mosi, kwa wakimbizi wenyewe, katika kutoa huduma za elimu, afya, kijamii, ulinzi, na kuwapa fursa ya kuishi. Ni muhimu kwa sababi UNRWA huchangia utulivu kwa kuwasaidia wakimbizi wa Palestina katika kanda yenye vurugu. Bila UNRWA, ni nani angewasaidia wakimbizi wa Palestina, jamii ambayo ni maskini, iliyo hatarini, lakini thabiti?”

Ban amesema ni dhahiri kwamba operesheni za UNRWA kwa ajili ya wakimbizi wa Palestina ni suala linalomgusa kila mtu. Hata hivyo, amesema chini ya miezi tisa tangu alipotoa wito kwa Baraza Kuu kuhusu usaidizi kwa UNRWA, shirika hilo limo tena katika uhitaji mkubwa wa rasilmali, na hivyo akatoa wito tena

“Nawahimiza kutafakari kuhusu suala la ubinadamu wa wakimbizi wa Palestina- matumaini yao, ndoto zao, na matamanio yao ya haki na utu. Kama ripoti yangu kwa Mkutano wa masuala ya kibinadamu duniani inavyosema, kuna ubinadamu mmoja na tuna wajibu wa pamoja wa kulinda, kuunga mkono na kuendeleza huo ubinadamu.”

image
Katibu Mkuu Ban Ki-moon akizungumza na wanafunzi wa shule za UNRWA kwa njia ya video kupitia mtandao wa intaneti. UNRWA, ambayo huendesha shule 700 katika maeneo ya Wapalestina yaliyokaliwa, pamoja na katika nchi za Jordan, Lebanon na Syria, sasa inakabiliwa na uhaba wa fedha ikihitaji dola milioni 81 kukidhi mahitaji ya wakimbizi wa Palestina. UN Photo/Rick Bajornas
Katibu Mkuu hakuishia hapo. Ameendelea kutoa ombi jingine la ufadhili

“Nawasihi leo mfanye kila muwezalo kusaidia na kuendeleza UNRWA na kazi yake. Upungufu wa sasa wa dola milioni 81 unapaswa kushughulikiwa kama jambo la kipaumbele kwa mwaka 2016.”