Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mateso dhidi ya vyama vya wafanyakazi yaongezeka Somalia

Mateso dhidi ya vyama vya wafanyakazi yaongezeka Somalia

Wataalam wa Umoja wa Mataifa wameisihi leo serikali ya Somalia kusitisha vitendo vya vitisho dhidi ya wanachama na viongozi wa vyama viwili vya wafanyakazi.

Vyama viwili hivyo ni Jumuyia ya vyama vya wafanyakazi vya Somalia (FESTU) na Chama cha kitaifa cha waandishi wa habari (NUSOJ).

Taarifa iliyotolewa leo inawanukuu watalaam hao wakisema serikali inapaswa kuheshimu haki ya kila mtu ya kujieleza huru, wakiwemo wanachama wa vyama vya wafanyakazi.

Aidha imeeleza kwamba Katibu Mkuu wa NUSOJ, Omar Faruk Osman, ameponea chupuchupu jaribio la kumwua mjini Mogadishu mwaka uliopita, na uchunguzi ulioanzishwa haukuhitimishwa.

Mbali ya hayo, mwezi Februari mwaka huu, bwana Osman ameshtakiwa kuwa anajaribu kuipaka matope serikali, na amekatazwa kusafiri wakati uchunguzi ukiendelea.

Halikadhalika taarifa inasema kwamba bwana Osman na viongozi wengine wa vyama hivyo wanaendelea kutishiwa na kunyanyaswa na serikali.

Vitendo hivyo vimefanyika licha ya mtalaam wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Somalia kuzuru nchi hiyo mapema mwaka huu na kuelezea wasiwasi wake kuhusu hali hiyo.

Baraza la Usalama linatarajia kutembelea Somalia mwezi huu, nchi hiyo ikiwa katika maandalizi ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Agosti mwaka huu.