Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Suala la Syria liwasilishwe ICC- Feltman

Suala la Syria liwasilishwe ICC- Feltman

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo limekumbushwa tena hoja ya kuwasilisha kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC mzozo wa Syria.

Mkuu wa masuala ya kisiasa kwenye Umoja wa Mataifa Jeffrey Feltman amerejelea wito huo wa Katibu Mkuu wakati akiwasilisha mbele ya baraza hilo hali halisi nchini Syria kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni kutoka vikosi vya serikali na upinzani kwenye mji wa Aleppo yaliyosabaisha vifo, majeruhi na mali kuharibiwa.

Amesema hali ni mbaya na kitendo cha kutumia njaa kama silaha ya vita hakikubaliki na hakiwezi kuhalalishwa kwa sababu yoyote ile…

“Nakumbusha wajumbe wa baraza juu ya wito wa Katibu mkuu wa kuwasilisha suala hili la hali ya Syria mbele ya mahakama ya kimataifa ha uhalifu. Wale wanaohusika na uhalifu wa kivita wawajibishwe.”

Kuhusu mwelekeo wa mchakato wa kisiasa kwa mujibu wa azimio la baraza la usalama namba 2254, wakati huu mazungumzo ya amani yakiwa vuta nikuvute, Bwana Feltman amesema Katibu Mkuu na mjumbe wake kuhusu Syria, Staffan de Mistura wanajaribu kupata mwelekeo ifikapo mwezi Agosti.

(Sauti ya Feltman)

“Hatuwezi kupoteza fursa hii ya mazungumzo Geneva. Kuruhusu pande kwenye mzozo kuchezea muda, au vikundi kujiimarisha maeneo yao na katika meza ya mazungumzo itakuwa ni kosa. Umoja wa Mataifa utajitahidi kurejesha mashauriano kadri iwezekanavyo huku kukiwa na matumaini kuwa juhudi za kurejesha sitisho la chuki ikiwemo Aleppo zitazaa matunda.”