Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP na OCHA zaimarisha ubia kuhusu uhakika wa kuwa na chakula

WFP na OCHA zaimarisha ubia kuhusu uhakika wa kuwa na chakula

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), zimetangaza kuwa zinaimarisha ubia katika kuelewa jinsi familia nchini Yemen zinavyohaha kukabiliana na kutokuwa na uhakika wa kupata chakula, kupitia ubadilishanaji na uwekaji wazi takwimu kupitia teknolojia ya simu. Taarifa kamili na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Takwimu hizo zinazokusanywa kupitia huduma ya WFP ya kufuatilia uhakika wa kuwa na chakula (mVAM), zinamulika matumizi ya chakula katika kila familia, na hivyo kuonyesha jinsi familia hizo zinavyojikimu wakati wa njaa na uhaba wa chakula kila mwezi.

Kutokana na takwimu hizo, kufikia mwezi Machi 2016, asilimia 70 ya familia katika kila mkoa wa Yemen ama zinakopa chakula, au kutegemea rafiki na jamaa zao katika kukabiliana na kutokuwa na uhakika wa kupata chakula. Kiwango ni kikubwa zaidi katika mikoa iliyoathiriwa moja kwa moja na mgogoro.

WFP na OCHA zinapanga kupanua mbinu hii ili kuonyesha takwimu kutoka nchi zingine.