Skip to main content

UM walaani shambulio dhidi ya msafara wa misaada ya kibinadamu Mali

UM walaani shambulio dhidi ya msafara wa misaada ya kibinadamu Mali

Kaimu mratibu wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA nchini Mali, amelaani vikali shambulio dhidi ya msafara wa misaada ya kibinadamu wa shirika lisilo la kiserikali la Danish Refugee Council (DRC) lililofanyika mwishoni mwa wiki.

Bi Fatouma Seid amesema shambulio hilo lilitokeo Kusini Magharibi mwa mji wa Gao na limefanywa na watu wasiojulikana ambao walianza kufyatulia risasi msafara huo,na wafanyakazi watatu wa misaada wamejeruhiwa mmoja vibaya sana na magari mawili kuwashwa moto.

Mratibu huyo amesema mashambulizi kama hayo yanatia hofu, na hayakubaliki hasa kuwalenga wafanyakazi wa misaada.

Ameongeza kuwa huo ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na ametoa wito wa wahusika lazima wafikishwe kwenye mkono wa sheria na kuwajibishwa ili haki itendeke.

Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea sanjari na hatua za kuchukua ikiwa ni pamoja na tathimini ya hatari kwa wafanyakazi wa misaada katika eneo lililoathirika.