Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kambi za walinda amani Sudan Kusini zatathminiwa

Kambi za walinda amani Sudan Kusini zatathminiwa

Tukiondoka tutauawa”, ni jina la ripoti huru mpya iliyotolewa leo kuhusu hali ya kibinadamu kwenye sehemu za ulinzi wa raia, PoC nchini Sudan Kusini ikisema kuwa zaidi ya watu 200,000 wamesaka hifadhi kwenye kambi za walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo na hadi sasa wanaendelea kuishi kwenye maeneo hayo.

Ripoti hiyo imeandaliwa kwa ushirikiano na serikali ya Uswisi na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM ili kutathmini hali ya kibinadamu kwenye sehemu hizo ambazo awali hazikulengwa kupokea wakimbizi wa ndani.

Mathalani ripoti imeonyesha kwamba sehemu hizo zimejaa kupitia kiasi na hali ya maisha ni ngumu, lakini bado ni suluhu ya pekee kwa maelfu ya watu ambao wamekimbia mashambulizi ya waasi.

Mashahidi wanaonukuliwa kwenye ripoti hiyo wanasema kwamba heri kuishi kwenye PoC kuliko kupoteza uhai nje ya maeneo hayo.

Mapendekezo ya ripoti hiyo ni kuimarisha ushirikiano na mashirika ya kibinadamu ili kuboresha hali ya maisha ndani ya kambi hizo.

Mzozo unaoendelea nchini Sudan Kusini umeshasababisha vifo vya watu zaidi ya 50,000, huku watu milioni 1.7 wakiwa wakimbizi wa ndani na wengine zaidi ya 700,000 wakiwa wametafuta hifadhi nje ya nchi.