Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lataka kulindwa kwa huduma za afya vitani

Baraza la Usalama lataka kulindwa kwa huduma za afya vitani

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekutana kujadili huduma za afya wakati wa vita, wakati ambapo hospitali zinaendelea kulengwa na mashambulizi na daktari kuuawa, hasa nchini Syria. Halikadhalika baraza limepitisha azimio kuimarisha ulinzi wa sekta hiyo. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Azimio lililopitishwa leo na Baraza la Usalama linaziomba pande za mzozo kote duniani kuheshimu sheria ya kimataifa ya kibinadamu na kujizuia kushambulia hospitali na wahudumu wa afya. Likilaani mashambulizi hayo, azimio hilo limeziomba serikali za nchi husika kuchukua hatua ili kuyazuia na kuadhibu washambuliaji.

Akihutubia Baraza hilo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema mara nyingi mashambulizi dhidi ya hospitali siyo ajali iliyotokea kwa bahati mbaya, bali ni lengo la washambuliaji, akiongeza kwamba mashambulizi ya aina hiyo ni uhalifu wa kivita.

Mwaka 2015, Bwana Ban amesema hospitali 34 zimeshambuliwa duniani kote, akitaja Syria, lakini pia Yemen, Afghanistan, Iraq na Sudan Kusini.

Bwana Ban ameeleza kwamba siku hizi pande za mzozo zinazidi kutoheshimu sheria ya kimataifa wakati wa vita, akikumbusha

(Sauti ya Bwana Ban)

“ Hata vita vina kanuni. Sasa ni wakati wa kuzilinda na kuzisimamia . Hakuna serikali inayopaswa kusalia kimya na kuangalia kanuni za ulinzi wa raia kwenye mizozo zinapuuzwa. Jamii ya kimataifa  kamwe haipaswi kunyamazia ukikukwaji zaidi uliowazi.”

image
Dkt. Joanne Liu, (kulia) mkuu wa MSF na Bw. Peter Maurer, (kushoto) Mkuu wa ICRC wakizungumza na wanahabari baada ya kuhutubia Baraza la Usalama. (Picha:UN/Rick Bajornas)
Kwa upande wake, mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la madaktari wasio na mipaka, Médecins sans Frontières, MSF, Daktari Joanne Lio, amekumbusha maadili ya udaktari, akitaja kiapo kinachofanywa na madaktari :

(Sauti ya Bi Liu)

« Tunahudumia kila mtu, bila kujali ni nani, bila kujali dini yake, kabila au upande gani anapopigana kwenye mzozo. Hata kama ni mpiganaji aliyejeruhiwa, au akitambuliwa kama muuaji au gaidi. Hospitali hazipaswi kushambuliwa au kuingiliwa kwa nguvu na askari, ikiwemo kusaka na kukamata wagonjwa. Kutelekeza maadili hayo ya msingi ni kutelekeza msingi wa maadili ya udaktari»

Bi Liu amekariri wito wake wa kusitisha mashambulizi hayo, na kunyoshea kidole wanachama wa baraza la Usalama, akisema

(Sauti ya Bi Liu)

« Mnawajibika kulinda amani na usalama. Lakini wanne kati ya wa wanachama watano wenye viti vya kudumu kwenye Baraza hili wameshiriki kwa kiwango mbalimbali kwenye miungano iliyotekeleza mashambulizi dhidi ya vituo vya afya mwaka uliopita. »

Naye Rais wa Kamati ya Kimataifa ya chama cha Msalaba Mwekundu, ICRC, Peter Maurer, amesisitiza kwamba vita vinaathiri maisha na afya ya raia wote, na mahitaji ya huduma za afya yanaongezeka zaidi, huku vituo vya afya vikizidi kushambuliwa.

image
Huduma za afya kwa watoto waliozaliwa njiti katika moja ya vituo vya afya kwenye mizozo. (Picha:UNICEF/Mohamed Yacine)
Akipongeza wanachama wa Baraza hilo kwa azimio lililopitishwa, akatoa mapendekezo kadhaa kuhusu jinsi ya kuimarisha ulinzi wa hospitali na wagonjwa wakati wa vita, akizingatia :

(Sauti ya Bwana Maurer)

« Leo, kwa azimio hili, mlikariri umuhimu wa sheria za vita, uelewa wa msingi ya kibinadamu iliyopitishwa na mikataba ya Geneva. wakidai iheshimiwe kupitia hatua za vitendo, ni hatua inayofuata ambayo Baraza hili linaweza kuchukua ili kuhakikisha ubinadamu kwenye vita ni dhahiri na siyo tu ndoto. »