Skip to main content

Idadi ya vifo Iraq imepungua kwa mwezi Aprili:UNAMI

Idadi ya vifo Iraq imepungua kwa mwezi Aprili:UNAMI

Jumla ya Wairaq 741 wameuawa na wengine zaidi ya 1300 kujeruhiwa katika mashambulizi ya kigaidi na vita nchini Iraq kwa mwezi wa A[pril mwaka huu, kwa mujibu wa takwimu zilizoorodheshwa na mpango wa msaada wa Umoja wa mataifa Iraq UNAMI.

Takwimu zinaonyesha idadi ya raia waliouawa ni 410 wakiwemo polisi 11, na waliojeruhiwa 973 wakiwemo polisi 20. Kwa ujumla watu zaidi ya 300 kutoka vikosi vya usalama pia wamepoteza maisha wakijumuisha Peshmerga, SWAT na wana mgambo wanaopigana kuisaidia serikali, huku waliojeruhiwa wakifikia zaidi ya 400.

UNAMI inasema kwa ujumla idadi ya vifo mwezi Aprili imeshuka kidogo ikilinganishwa na mwezi Machi ambao ulishuhudia watu zaidi ya 100 wakipoteza maisha na zaidi ya 1500 waliojeruhiwa.

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa mataifa na mkuu wa UNAMI nchini Iraq Ján Kubiš, ameelezea hofu yake kuhusu ghasia zinazoendelea na kuongeza kuwa magaidi wametumia mashambulizi ya kujitoa muhanga kwenye migahawa, maeneo ya kuabudu, mahujaji na masokoni kuhakikisha wanakatili maisha ya watu wengi zaidi.