Skip to main content

Haki ya kupata habari hutegemea uhuru wa vyombo vya habari- Ban

Haki ya kupata habari hutegemea uhuru wa vyombo vya habari- Ban

Kuelekea siku ya uhuru wa vyombo vya habari hapo kesho Mei 3, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amesema haki za binadamu, jamii zenye demokrasia na maendeleo endelevu vinategemea usambazaji huru wa habari. Taarifa kamili na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Katika ujumbe wake, Ban amesema haki ya kupata habari hutegemea uhuru wa vyombo vya habari.

Kwa mantiki hiyo, Katibu Mkuu amesema maadhimisho ya kesho ni fursa ya kusisitiza kanuni hizi muhimu, kulinda uhuru wa vyombo vya habari, na kuwaenzi wanahabari ambao huhatarisha na wakati mwingine kupoteza maisha wakati wakifanya kazi yao.

Aidha, Ban amesema maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika katika mwaka wa kwanza wa malengo ya maendeleo endelevu, na kwamba uhuru wa vyombo vya habari ni muhimu siyo tu kwa kuwaelewesha raia kuhusu malengo hayo, lakini pia kuwawezesha kuwawajibisha viongozi wao kutimiza ahadi walizoweka.