Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akaribisha uteuzi wa mawaziri katika serikali ya mpito Sudan Kusini

Ban akaribisha uteuzi wa mawaziri katika serikali ya mpito Sudan Kusini

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amekaribisha uteuzi wa mawaziri wa serikali ya mpito nchini Sudan Kusini, kulingana na makubaliano ya Agosti 17 2015 ya kuutanzua mgogoro nchini humo.

Akikaribisha uteuzi huo uliofanywa na Rais Salva Kiir, Katibu Mkuu amesema amefurahi kuona kwamba Rais Kiir na Makamu wake Riek Machar wamefikia hatua hii muhimu ya mchakato wa amani, na kutoa wito wakamilishe hima uundaji wa taasisi zote za mpito.

Aidha, taarifa ya msemaji wake imesema kuwa Ban ametoa wito kwa pande zote zikomeshe mara moja uhasama wote.

Msemaji wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS,  Arianne Quentier, ameeleza hatua zitakazofuata uteuzi wa baraza la mawaziri

“Kuna hatua kadhaa ambazo serikali inapaswa kuchukua. Kwanza ni kushughulikia suala la majimbo na kuteua kamisheni ya mipaka. Jingine linalopaswa kushughulikiwa na serikali ni uchumi uliozorota. Nchi hii imeathiriwa na vita. Hakuna uchumi tena, kuna mdororo mfumko mkubwa wa bei za bidhaa, watu hawawezi kufikia masoko. Watu anahitaji usaidizi wa kibinadamu. Tatu niraia kuweza kurejea majumbani kwao,  ambayo yameharibiwa. Itakuwa vigumu sana kuijenga tena nchi, lakini ni lazima kutendeke ili watu warejee nyumbani.”

Halikadhalika, Katibu Mkuuu amepongeza mwenyekiti wa Kamisheni ya ufuatiliaji na tathmini, Rais mstaafu Festus Mogae, na Mwakilishi Mwandamizi wa Muungano wa Afrika, Alpha Omar Konare, kwa kuusongesha mchakato wa amani mbele, na kukariri dhamira ya Umoja wa Mataifa kuunga mkono watu wa Sudan Kusini katika kurejesha amani, utulivu na ufanisi nchini mwao.