Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu wenye ulemavu wa ngozi Malawi hatarini kutoweka- Mtaalamu

Watu wenye ulemavu wa ngozi Malawi hatarini kutoweka- Mtaalamu

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wenye ulemavu wa ngozi, au albino, Ikponwosa Ero ameonya kuwa machungu na vitisho vinavyokabili albino nchini Malawi vinahatarisha uwepo wao iwapo hatua hazitachukuliwa.Taarifa kamili na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Akizungumza baada ya ziara yake rasmi ya kwanza nchini humo Bi. Ero amesema walemavu wa ngozi huko Malawi wanaishi kwa hofu kubwa, hawalali na hata hawaamini wale wanaopaswa kuwalinda kutokana na familia kuhusika katika baadhi ya matukio ya wao kushambuliwa.

Bi. Ero amesema hali ni mbaya zaidi kwa kuwa tangu mwaka 2014 visa 65 vya mashambulizi dhidi ya albino viliripotiwa nchini Malawi ikiwemo visa viwili wakati wa ziara yake.

Amesema fikra potofu za matumizi ya viungo vya albino kwa ushirikina na kwamba albino hawafariki dunia bali wanatoweka zinahatarisha zaidi maisha yao.

Pamoja na kupongeza mpango wa serikali wa mwaka 2015 kulinda albino, bado ametaka mafunzo zaidi kwa polisi, waendesha mashtaka na mahakimu ili hukumu za kesi hizo ziendane na ukubwa wa tukio husika.