Ban alaani mashambulizi dhidi ya hospitali Aleppo

28 Aprili 2016

Wakati mashambulizi ya anga kwenye hospitali ya Al Quds huko Aleppo Syria yaripotiwa kusababisha vifo vya watu wapatao 20, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amerejelea wito wake kuwa mzozo nchini humo hautamalizika kwa mtutu wa bunduki.

Taarifa ya msemaji wake imemnukuu akituma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha na waliojeruhiwa huku akilaani mashambulizi holela yanayofanywa na upande wa serikali na wapinzani.

Ban ametoa wito kwa pande hizo kumaliza chuki baina yao akitoa wito kwa wenyeviti wenza wa kikundi cha usaidizi kwa Syria, ISSG ambao ni Marekani na Urusi kushinikiza pande hizo kuacha mapigano na kuchunguza matukio kama hayo ya Al Quds.

Katibu Mkuu amesema bado anashawishika kuwa makubaliano yatakayokwenda sanjari na makubaliano ya Geneva mwaka 2012 na azimio namba 2254 la mwaka 2015 ndiyo yanayoweza kuleta suluhu ya mzozo wa Syria.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter