Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO na OIE zahaha kukwamua mbuzi na kondoo dhidi ya PPR

FAO na OIE zahaha kukwamua mbuzi na kondoo dhidi ya PPR

Ugonjwa hatari unaoshambulia mifugo aina ya mbuzi na kondoo, PPR umeendelea kuwa tishio duniani na sasa umeripotiwa katika nchi 76.

Kwa mujibu wa shirika la chakula na kilimo duniani, FAO, na lile la afya ya wanyama, OIE, ugonjwa huo unaoenezwa na kirusi sasa umeripotiwa huko Georgia, na hata Maldives huku ukiwa umeenea kwa kasi kwa miongo miwili sasa kwenye kanda za Afrika, Asia na Mashariki ya Kati.

Kaya za vijijini ambazo hutegemea zaidi mifugo hiyo kwa lishe, mbolea na sufi zimeathirika zaidi wakati huu ambapo ugonjwa huo unasababisha hasara ya dola Bilioni Mbili kwa mwaka.

Dkt. Juan Lubroth, mkuu wa kitengo cha magonjwa ya wanyama kutoka FAO anaelezea mikakati ya kutokomeza PPR..

(Sauti ya Dkt. Lubroth)

“Mosi, unajikita katika PPR kwa upande wa mbuzi na kondoo, chanjo na kufahamu mfumo mzima wa kuongeza thamani za mazao yao ili kuweza kuchukua hatua sahihi. Pili, ni kuimarisha huduma kwa mifugo na tatu unaangalia magonjwa mengine ya kipaumbele ambayo yanaweza kukabiliwa sambamba na PPR.”