Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tegemeo la maisha kwa mamilioni ya Wasyria liko hatarini:Egeland

Tegemeo la maisha kwa mamilioni ya Wasyria liko hatarini:Egeland

Machafuko yanayoendelea katika baadhi ya sehemu za Syria ni mabaya kama ilivyokuwa kabla ya usitishaji uhasama kuanza kutekelezwa , na hivyo kutishia mustakhbali wa mamilioni ya watu umesema Umoja wa Mataifa Alhamisi.

Jan Egeland, ambaye ni mratibu wa masuala ya kibinadamu wa kikosi kazi kwa ajili ya taifa hilo lilolosambaratishwa na vita, amesema zaidi ya nusu ya watu walio katika maeneo yaliyozingirwa , sasa wamefikiwa na ni zaidi ya watu 250,000, lakini ameonya kwamba mafanikio hayo huenda yakatoweka endapo mapigano yanaendelea, akitolea mfano miji ya Homs na Aleppo ambako daktari wa mwisho wa watoto ameuawa leo.

(SAUTI YA EGELAND)

"Zahma ni kubwa kwani maisha ya mamilioni ya raia yako hatarini, wafanyakazi wengi wa masuala ya kibinadamu wa afya na wafanyakazi wa misaada wanashambuliwa kwa mabomu, kuuawa, kupata vilema wakati huu,hivyo kwa ujumla hatima ya maisha kwa mamilioni ya watu pia iko hatarini."

Hadi sasa mwaka huu , Umoja wa Mataifa na washirika wake wamefikia karibu watu 800,000 katika maeneo yanayozingirwa ambayo ni magumu kufikika.