Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zeid alaani msururu wa mauaji Burundi:

Zeid alaani msururu wa mauaji Burundi:

Kamishina mkuu wa haki za binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein Jumatano amelaani vikali ongezeko la idadi ya mashambulizi dhidi ya maafisa wa ngazi za juu nchini Burundi , ikiwa ni pamoja na mauaji ya karibuni ya brigedia jenerali Athanase Kararuza na mkewe yaliyotokea Jumatatu, na pia jaribio la mauaji dhidi ya waziri wa haki za binadamu, ustawi wa jamii na jinsia, Martin Nivyabandi, Jumapili ya Aprili 24.

Zeid amesema ni lazima yafanyiwe uchunguzi wa kina na wauawaji wakamatwe na kufikishwa mbele ya sheria. Kwa mwezi huu wa Aprili watu 31 wameshauawa katika mashambulizi hadi sasa ikilinganishwa na watu tisa waliouawa mwezi uliopita.

Ameongeza kuwa mashambulio mengi yanafanywa na watu wenye silaha wasiojulikana na anatiwa hofu ya kuongezeka kwa idadi ya mauaji ya kupangwa ambayo yatachochea hatari ya ghasia Burundi ambayo hali bado ni tete.

Zeid amezichagiza pande zote Burundi kutumia fursa ya mazungumzo ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki yatakayoongozwa na Burundi mjini Arusha Tanzania , kujihusisha katika majadiliano kwa lengo la kuboresha hali ya haki za binadamu na kupata suluhu ya kudumu ya mgogoro wa kisiasa unaondelea nchini humo.