Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban apongeza azimio kuhusu ujenzi wa amani

Ban apongeza azimio kuhusu ujenzi wa amani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amepongeza nchi wanachama wa umoja huo kwa matokeo ya tathmini ya mfumo wa shughuli za ujenzi wa amani iliyowezesha kupitishwa kwa maazimio mawili hii leo na vyombo vikuu vya Umoja huo.

Ban ametoa kauli hiyo baada ya vyombo hivyo viwili vya Umoja wa Mataifa ambavyo ni Baraza Kuu na Baraza la Usalama kupitisha kwa pamoja maazimio yanayolenga kuboresha ujenzi wa amani hasa baada ya mizozo.

Stephane Dujarric ni msemaji wa Umoja wa Mataifa.

“Maazimio haya yanaashiria nia ya mabadiliko katika mikakati na fikra. Umoja wa Mataifa unafanya kazi kimkakati kwa ushirikiano na serikali kwenye nchi husika pamoja na wadau wengine siyo tu kuzuia kutokea mizozo mara kwa mara bali pia kuzuia mizozo hiyo isitokee.”

Ban ameahidi ushirikiano wa mfumo wa Umoja wa Mataifa katika kutekeleza maazimio hayo haraka iwezekanavyo akisema kuwa hakuna kipaumbele zaidi ya kuendeleza amani ambayo ni msingi katika kusimamia haki za binadamu na maendeleo endelevu.