Skip to main content

Ufilipino yatumia ‘drones’ kupunguza athari za majanga

Ufilipino yatumia ‘drones’ kupunguza athari za majanga

Nchini Ufilipino, shirika la chakula na kilimo duniani, FAO kwa kushirikiana na serikali wameanza kutumia ndege zisizo na rubani, Drones, kwa ajili ya kukabiliana na kuhimili athari za majanga kama vile mafuriko na vimbunga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi.

FAO inasema katika mradi wa sasa wa majaribio ndege mbili zisizo na rubani zinatumika kutathmini athari kwenye maeneo yaliyokumbwa na El nino na kazi yake ni kutathmini hali halisi kabla janga halijatokea na baada ili kuepusha uhaba wa chakula majanga yanapotokea.

Christopher Morales ni mkurugenzi wa kitengo cha huduma za ugani za kilimo nchini Ufilipino.

(Sauti ya Christopher)

“Tofauti na awali ambapo tulitumia takwimu kutoka kwa wadau wetu ambazo wakati mwingine zilikuwa makadirio ya juu au chini, hivi sasa kwa kutumia drones tunaweza kuwa na mbinu mahsusi kuchambua taarifa hizi na kuwa na mikakati sahihi wakati wa majanga.”

Mathalani ndege hizi zisizo na rubani kupiga picha kutoka angani na kuonyesha hali halisi ikiwemo maeneo ambako miundombinu ya kilimo kama vile umwagiliaji inaweza kuharibiwa na majanga au kujengwa na hivyo hatua sahihi kuchukuliwa kwa manufaa ya wakulima.