Athari za El Nino zinasisitiza haja ya maandalizi- UNISDR
Dunia inahitaji jitihada zaidi kukabiliana na athari za msimu mbaya zaidi wa El Nino kuwahi kutokea katika kipindi cha miongo mitano.
Hayo yamesemwa na maafisa wa misaada na maendeleo , wakihimiza wito wa maandalizi kwa kuzingatia mkakati wa upunguzaji hatari ya majanga wa Sendai.
Shirika la Umoja wa mataifa la upunguzaji hatari ya majanga UNISDR limesema watu milioni 60 wameathirika na El nino na fedha zaidi ya dola bilioni 3 zinahitajika ili kuwasaidia waathirika, lakini limetoa wito wa kuwa na maandalizi zaidi ili kujihami na zahma kama hii katika siku za usoni.
Katika miezi michache iliyopita serikali, Umoja wa mataifa na makundi ya misaada yamekuwa yakiongeza juhudi za mipango ya maandalizi na pia kukabiliana na athari za El nino.
Mtazamo wa hali ya hewa unaonyesha kwamba huenda hali ikawa mbaya zaidi kwani El nino na La Nina huenda vikakumba mwishoni mwa mwaka na kusababisha mafuriko, katika jamii ambazo zinakabiliwa na ukame Afrika na kuleta kimbunga Asia na Pacific.