Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bashua wa Nigeria kuongoza uchunguzi maalum wa mauaji Malakal

Bashua wa Nigeria kuongoza uchunguzi maalum wa mauaji Malakal

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amemteua Abiodun Oluremi Bashua wa Nigeria kuongoza jopo la uchunguzi maalum wa mashambulizi dhidi ya kituo cha kuhifadhi raia cha ujumbe wa Umoja huo nchini Sudan Kusini, UNMISS.

Kituo hicho kilichopo Malakal, kilishambuliwa tarehe 17 na 18 mwezi Februari mwaka huu ambapo raia wapatao 25 waliokuwepo kwenye kituo hicho waliuawa na wengine 144 walijeruhiwa.

Taarifa ya msemaji wa  Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa uchunguzi huu maalum utaunganishwa na ule uliofanywa na bodi maalum kutoka makao makuu ya Umoja wa Mataifa ambayo iliteuliwa tarehe 11 mwezi uliopita wa Machi.

Bwana Bashua hadi uteuzi huu alikuwa amekamilisha jukumu lake la Naibu mwakilishi wa ujumbe wa pamoja wa Umoja  wa Mataifa na Muungano wa Afrika, AU huko Darfur, Sudan.