Ban alaani mauaji ya Jenerali Burundi na familia yake

Ban alaani mauaji ya Jenerali Burundi na familia yake

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani mauaji ya Brigedia-Jenerali Athanase Kararuza, pamoja na mkewe na binti yake, mauaji yaliyotokea Burundi kwenye mji mkuu Bujumbura.

Wakati wa uhai wake, Brigedia Jenerali Kararuza alihudumu katika nafasi andamizi ndani ya uliokuwa ujumbe wa Afrika huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, MISCA na hata ulipokabidhiwa kwa Umoja wa Mataifa, MINUSCA.

Ban ametuma salamu za rambirambi kwa wale wote walioathirika kutokana na kifo cha afisa huyo wa jeshi akiongeza kuwa mauaji ya Brigedia-Jenerali Kararuza yamefanyika wakati katika wiki za karibuni nchini Burundi kumekuwepo na matukio mengi ya mauaji yanayochochewa kisiasa, ikiwemo shambulio la jana dhidi ya waziri wa haki za binadamu Martin Nivyabandi na maafisa wengine waandamizi wa kijeshi.

Amesema visa vyote hivyo havisaidii lolote zaidi ya kuzidisha hali ambayo tayari ni tete nchini Burundi. Katibu Mkuu anataka uchunguzi wa haraka na wa kina ufanyike dhdi ya matukio haya.

Katibu Mkuu amesisitiza ghasia zozote hazitaleta amani na suluhu pekee ni kupitia mchakato wa kisiasa kwa wananchi wa Burundi ili nchi yao irejee katika mwelekeo wa maridhiano ya kitaifa na amani.

Ametoa wito kwa viongozi wote wa kisiasa ikiwemo wale walioko ughaibuni kukataa ghasia wanaposongesha malengo yao ya kisiasa na badala yake waazimie mazungumzo shirikishi.