Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Real Madrid yapeleka mradi wa shule na michezo Gaza

Real Madrid yapeleka mradi wa shule na michezo Gaza

Wafanyakazi wa Shirika la Hisani la timu ya kandanda ya Real Madrid kutoka Uhispania, wamekuwa Mashariki ya Kati tangu Aprili 23 hadi leo Aprili 25, kufanikisha mradi wa pamoja wa kijamii na Shirika la Umoja wa Mataifa linalowasaidia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).

Mradi huo wa shule za kijamii na michezo unalenga kunufaisha watoto katika maeneo ya Wapalestina yaliyokaliwa.

Chini ya mradi huo ambao umekuwa ukiratibiwa tangu mwaka 2011, shirika hilo la hisani la Real Madrid Foundation limeweka ahadi mpya ya dhamira ya kuhakikisha kuwa watoto wakimbizi wa Kipalestina wanakwenda kusoma katika shule za UNRWA katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi.

Taarifa ya UNRWA imesema kuwa michezo na mazoezi mengine ya kijamii ni muhimu hata zaidi wakati huu, kutokana na hali wanayokabiliwa nayo watoto katika Ukanda wa Gaza, kufuatia uhasama wa mwaka 2014, na kwamba mazoezi ya kijamii na michezo itawasaidia watoto hao kupata ahueni kutokana na uchungu waliokumbana nao wakati wa mapigano ya kijeshi.